Vita dhidi ya ujangili inazidi kushika kasi baada ya kikosi kazi maalumu cha kupambana na ujangili kumnasa Mhifadhi Mwandamizi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) kwa tuhuma za ujangili.
Pia, kikosi hicho kimemtia mbaroni Mchungaji wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), wilayani Arumeru kwa tuhuma za kukutwa na jino la tembo wakati akisaka mnunuzi.
Waziri wa Utalii na Maliasili, Profesa Jumanne Maghembe alisema jana kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimeongeza kasi ya kupambana na majangili katika mapori yote ya akiba.
Meneja Uhusiano wa Tanapa, Paschal Shelutete katika taarifa yake jana alisema kuwa Mei 14, mwaka huu, shirika hilo lilipokea taarifa za siri kuwa mchungaji huyo alikuwa akimiliki jino hilo.
“Tuliambiwa mchungaji huyo alikuwa akihitaji mtu wa kufanya naye biashara. Baada ya kupata taarifa tuliwasiliana na kikosi kazi maalumu cha kitaifa ili wafuatilie,” alisema Shelutete.
Shelutete alidai kuwa Mei 15, mchungaji huyo alikamatwa na kumtaja ofisa wa Tanapa kuwa ni mmoja wa washirika wake katika biashara hiyo.
“Alipokamatwa na kuhojiwa alimtaja mhifadhi huyo kuwa anataarifa za yeye kuwa na jino hilo ndipo Mei 16 naye alikamatwa,” alisema Shelutete.
Tanapa imewaomba raia wema kuendelea kufichua vitendo vya ujangili na haitasita kuchukua hatua dhidi ya watumishi wake watakaobainika kujihusisha na ujangili.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Waziri Maghembe alisema majangili sasa wamehamishia ujangili wao katika mapori ya akiba baada ya kudhibitiwa kwa kiasi kikubwa katika Hifadhi.
Profesa Maghembe alionya kuwa hakuna jangili hata mmoja ambaye atasalimika katika msako unaoendelea na kwamba, salama yao ni kujisalimisha pamoja na silaha zao.
Kukamatwa kwa ofisa huyo mwandamizi wa Tanapa kumekuja miezi michache baada ya kufikishwa mahakamani kwa Mkuu wa Kitengo cha Intelijensia cha Mamlaka ya Ngorongoro kwa tuhuma za ujangili.
Mtuhumiwa huyo, Iddy Mashaka (49), anadaiwa kuwa Januari 6 na Februari Mosi wilayani Meatu alimshauri mshtakiwa namba mbili, Shija Mjika (38) kuua wanyama wasioruhusiwa.
Watuhumiwa wengine ambao wanashitakiwa pamoja na Mkuu huyo wa Kitengo cha Intelijensia, wao wameshitakiwa kwa kutungua helkopta na kumuua rubani wake, Rogers Gower huko Maswi.